http://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/issue/feedJarida la Dira ya Lugha2025-05-08T11:57:13+03:00Jarida la Dira ya Lugha, Idara ya Isimu, Lugha na Fasihi, Chuo Kikuu cha South Eastern Kenya,jadilu@seku.ac.keOpen Journal Systems

Jarida la Dira ya Lugha (JADILU) lilianzishwa mwaka 2023. Hili ni jarida la kimataifa linalochapisha makala zake mara mbili kwa mwaka. JADILU ni jarida linalolenga kuchochea mijadala inayohusu Taaluma za Kiswahili zikiwemo isimu, lugha, fasihi pamoja na taaluma zinazohusiana nazo kama vile tafsiri na ukalimani. Jarida hili ni njia muhimu ya kusambaza maarifa yanayoibuliwa na tafiti mbalimbali za taaluma za Kiswahili. Jarida linapatikana katika nakala ngumu pamoja na nakala tepe ya mkondoni.

Lengo kuu la JADILU ni kukuza, kueneza na kutandawaza lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Mswahili na Mwafrika. Hivyo, tunahimiza wanazuoni, watafiti na wataalamu mbalimbali kutuma makala za taaluma zote za Kiswahili, Tafsiri, Ukalimani na Utamaduni wa Kiswahili kutoka kote duniani kuchapishwa katika jarida la Dira ya Lugha. Tunapokea miswada iliyoandikwa kwa Kiswahili na Kiingereza na inayohusu taaluma za Kiswahili na Kiafrika.

http://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/31Athari za Matamshi ya Lugha za Jamii na Ukiushi wa Maana katika Kiswahili Sanifu2025-05-08T11:57:13+03:00Ahmad Yahya Sovusovu82@gmail.com
Makala hii imechunguza athari za matamshi ya lugha za jamii zinavyosababisha ukiushi wa maana katika maneno ya Kiswahili Sanifu. Hoja kuu katika makala hii ni kuwa, pamoja na kuwapo kwa tafiti anuwai zilizodhihirisha vipengele mbalimbali vya matamshi vilivyotokana na kuathiriana kati ya lugha za jamii na Kiswahili, bado kwa kadri ya uelewa wetu hakuna tafiti zilizobainisha athari za ukiushi wa maana za maneno zinazotokana na kuathiriana kati ya lugha hizo. Data za msingi katika makala hii zimekusanywa maktabani na uwandani kwa kutumia mbinu za usomaji makini na mahojiano. Matokeo ya uchunguzi yanaonesha kwamba kuna vipengele mbalimbali vya matamshi katika lugha za jamii vinavyoathiri maana katika matumizi ya Kiswahili Sanifu. Mathalan, matumizi ya sauti [f] badala ya [v], [a] badala ya [h], [bh] badala ya [b] na [l] badala ya [r] na kinyume chake. Athari za matumizi ya sauti hizo ni kubadilisha matamshi, udondoshaji na kuathiri maana za maneno, katika Kiswahili Sanifu. Pia huchangia kuibuka kwa maneno ambayo hayafahamiki kabisa katika Kiswahili Sanifu. Makala hii inatoa mchango kwa watumiaji wa Kiswahili wageni na hata wenyeji wanaojifunza lugha ya Kiswahili kufahamu Kiswahili Sanifu na maana za maneno kwa usahihi wake. Hivyo, ni muhimu kuzingatia matamshi sahihi ya maneno ya Kiswahili Sanifu kwani matamshi yana mfungamano mkubwa na maana za maneno. Kutokana na hali hiyo, ndio maana kubadili sauti katika matamshi ya maneno kunabadili pia maana halisi za maneno yaliyokusudiwa.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/30Nafasi ya Picha katika Kukuza Upokezi wa Msomaji katika Vitabu Teule vya Fasihi ya Watoto2025-05-08T09:16:01+03:00Silvester L. Makaumakau.silvester@yahoo.comPamela M. Y. Ngugingugi.pamela@ku.ac.ke
Makala hii imelenga kubainisha nafasi ya picha katika kukuza upokezi wa msomaji katika vitabu teule vya fasihi ya watoto: Kesho! Kesho! (Hussein, 2009) na Werevu wa Juma (Yahya, 2003). Utafiti huu umechochewa na kuwepo kwa pengo kuhusu jinsi picha hukuza upokezi wa msomaji hususan katika hadithi za Kiswahili teule. Makala hii imeongozwa na Nadharia ya Mwitikio wa Msomaji.Muundo wa utafiti huu umekuwa wa kimaelezo na kitakwimu. Data zilikusanywa kwa kusoma na kuchanganua makala na vitabu teule, pamoja na njia ya mahojiano na wanafunzi wa shule za msingi waliopo ngazi ya gredi ya pili. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa upokezi wa ujumbe huimarishwa ikiwa msomaji atatambua vigezo muhimu katika picha. Vigezo hivi ni kama vile: Mtafitiwa kutambua picha kwenye kitabu polepole ama kwa haraka, kutambua wahusika, rangi na mandhari, kuchanganua ujumbe wa picha kutumia vigezo vya mandhari, ishara, maandishi kwa picha, rangi, nyuso za wahusika na mavazi, upokezi wa ujumbe usiofanana na unaofanana kwenye picha na matini, watafitiwa kufanya masimulizi kulingana na ujumbe walioupokea kutokana na picha kwenye vitabu teule, upokezi kutokana na umilisi, mshikamano na mtiririko wa hadithi, mafunzo ya picha kutokana na upokezi wa ujumbe kwenye picha na matini, kubaini dhima ya picha kulingana na upokezi wa ujumbe katika picha, umakini katika kusoma na kung’amua maandishi na kujadili uhusiano wa picha na maandishi, hali ya nyuso zilizofurahia na zilizo na huzuni kama kigezo cha hisia.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/29Changamoto katika Ubidhaishaji wa Kiswahili Nchini Tanzania2025-05-08T08:52:33+03:00Elishafati J. Ndumiwendumiweelisha@gmail.comZacharia Madilazamadila9@gmail.com
Lugha ya Kiswahili imekuwa bidhaa adimu kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na fursa za ajira zinazopatikana ndani yake (Mahenge, 2021). Miongoni mwa fursa hizo ni tafsiri, ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, ufundishaji wa Kiswahili nje ya nchi na uandishi na uchapishaji wa nyaraka za Kiswahili. Wadau mbambali nchini Tanzania wamechangamkia fursa hizo ili kunufaika kiuchumi. Hata hivyo, zipo changamoto zinazojitokeza katika kunufaika na fursa zilizopo katika lugha ya Kiswahili nchini Tanzania. Kwa hiyo, lengo la makala hii ni kuchunguza changamoto katika ubidhaishaji wa Kiswahili na kupendekeza njia za kutatua changamoto hizo. Data za makala hii zimekusanywa Jijini Mwanza katika kongamano la wadau wa Kiswahili. Watoa taarifa 36 walihusika katika kutoa data za utafiti huu. Watoa taarifa hao waliteuliwa kwa kutumia usampulishaji lengwa. Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data ni hojaji na usaili. Aidha, uwasilishaji wa data ulitumia mbinu ya maelezo. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa ubidhaishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania hukumbwa na ubeberu wa lugha za kigeni katika Kiswahili, dhana potofu kuhusu lugha ya Kiswahili, utamaduni hafifu wa kujisomea, kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu ajira nje ya nchi, uhusikaji wa wasiowataalumu katik shughuli za taaluma za Kiswahili na ufinyu wa soko la ajira nje na ndani ya nchi. Vilevle, makala imebainisha kuwa, mbinu za utatuzi wa changamoto hizo ni uimarishaji wa mafunzo kwa walimu wa Kiswahili kwa wageni, BAKITA kutoa leseni kwa taasisi au watu wanaojishughulisha na taaluma za Kiswahili kama vile wafasiri, wakalimani na watoamafunzo ya Kiswahili kwa wageni.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/28Viswahili na Wahaka wa Kiisimu: Haja ya Kupanua Rajamu ya Kiswahili2025-05-08T08:46:17+03:00Peter Githinjipeter.githinji@ku.ac.ke
Tunapokaribia karne moja ya usanifishaji wa Kiswahili, ni dhahiri kuwa ni wachache wanaoongea Kiswahili Sanifu katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati. Hili linatokana na kuwa idadi kubwa ya wakazi wa ukanda huu hujifunza Kiswahili kama lugha ya ziada, huku uhawilisho wa vipengele vya lugha mzazi ukisababisha kuwepo kwa lafudhi mbalimbali. Unyanyapaa wa Viswahili vyenye lafudhi huwapa wasemaji wengi au wazungumzaji watarajiwa kujitilia shaka wanapozungumza Kiswahili. Makala hii inaangazia wahaka wa kiisimu unaowafanya wakazi wa baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki kuambaa kuongea Kiswahili au kupendelea Kiswahili chenye utosarufi. Inapigia debe rajamu pana ya Kiswahili itakayosherehekea tofauti za wazungumzaji katika kupanua matumizi ya Kiswahili. Vilevile inasisitiza kupanuliwa kwa mikabala ya taaluma ya elimulahaja ya Kiswahili ili ijumuishe Viswahili vya kimaeneo vinavyoakisi uhalisia wa sehemu zote kinakozungumzwa. Makala hii inahitimisha kwa kutoa wito wa kufanya utafiti zaidi kuhusu wahaka wa kiisimu ili kuondoa ubaguzi wa kiisimu unaotokana na unyanyapaa. Hili ndilo litakalofanya rajamu ya Kiswahili imilikiwe na ikubalike na watu wote wanaozungumza Kiswahili.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/27Ontolojia ya Nafsi katika Riwaya Teule za Muhammed Said Abdulla: Uchunguzi wa Kikani2025-05-08T08:41:41+03:00Tatu Y. Khamiskhamist910@gmail.comArafa Jumannearafajay@gmail.com
Makala hii inajadili ontolojia ya nafsi katika riwaya teule za Muhammed Said Abdulla kwa kujiegemeza katika kipengele cha kani. Kimsingi, kila mwanadamu ana nafsi. Nafsi ni kipengele kinachotazamwa kama uhai, roho pamoja na moyo (Kaponda, 2018). TUKI (1981) wanafasili dhana ya nafsi kuwa ndiyo roho au kiini cha dhati ya jambo husika. Hivyo, nafsi huongoza hali ya kupumua na kuupa uhai mwili wa mwanadamu. Aidha, kila nafsi inaongozwa na kani ambayo aghalabu huwa ni fiche. Data za msingi zilizofafanuliwa katika makala hii zimepatikana maktabani na uwandani kwa kutumia mbinu ya usaili na uchambuzi wa maandiko. Nadharia ya Nje- Ndani ilitumika katika kuongoza mjadala. Matokeo ya mjadala yanaonesha kuwa nafsi kiontolojia haiwezi kuonekana lakini kani yake inabainika katika matendo, lawama, kupaparika, kutulia na kuamrisha maovu. Ithibati ya matokeo haya yametolewa kutoka katika riwaya tatu za Muhammed Said Abdulla ambazo ni Duniani Kuna Watu, Kosa la Bwana Msa, na Kisima cha Giningi.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/26Utohoaji na Matumizi ya Maneno Changamani katika Lugha ya Kiswahili: Mifano ya Mkanganyiko wa Maana na Matumizi ya Neno “Bongofleva” Nchini Tanzania2025-05-08T08:35:05+03:00Issaya Lupogoissaya.lupogo@mu.ac.tz
Lugha ya Kiswahili kama zilivyo lugha zingine ina kawaida ya kutohoa maneno kutoka lugha mbalimbali. Miongoni mwa maneno yanayotoholewa ni maneno changamani, yaani neno moja linaloundwa na maneno zaidi ya moja; mfano, neno Bongofleva (lililotokana na kirai cha Kiingereza Bongo Flavour). Kumekuwa na mkanganyiko wa mawazo kuhusu maana ya Bongofleva na mwasisi wa neno hilo. Makala hii inaonesha mawazo mbalimbali yanayokinzana kuhusu masuala hayo mawili. Makala hii ni matokeo ya mapitio ya maandiko na tajiriba ya mwandishi katika uga wa muziki wa Bongofleva akiwa mdau, mfuatilitiaji, mchambuzi na msanii wa muziki huo. Aidha, sehemu ya data zilishadidiwa kwa kufanya mahojiano na msanii na mtangazaji wa zamani aitwaye KCB. Makala hii imebaini kwamba jina “Bongofleva” liliasisiwa na kutumiwa kwa mara ya kwanza na Mhagama Pesambili (aliyewahi kuwa mtangazaji wa Radio One) na KCB katika kipindi cha DJ Show. Kuhusu maana ya Bongofleva, makala inapendekeza kwamba aina zote za miziki zinazopatikana nchini Tanzania zipo chini ya mwamvuli (kapu) wa Bongofleva kwa kujikita katika mantiki kwamba Bongofleva ni neno lililotoholewa kutoka katika lugha ya Kiingereza “Bongo Flavour” likiwa na maana ya msingi ambayo ni ladha kutoka Bongo/Dar/Tanzania.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/25Usambamba wa Kisemantiki Kati ya Methali za Kikuyu na za Kiswahili2025-05-08T08:27:49+03:00Esther Chombaechomba@seku.ac.ke
Makala hii imeshughulikia usambamba wa kisemantiki kati ya methali za Kikuyu na za Kiswahili kwa kuangazia methali zinazobainisha nafasi ya mwanamke, ndoa na malezi katika jamii hizi. Lengo kuu lilikuwa kuchanganua methali zilizoteuliwa kimakusudi ili kubainisha usambamba wa kimaana unaodhihirika na mtazamo wa wanajamii hawa kuhusu mahusiano ya kimapenzi, ndoa na malezi. Methali nane zimeteuliwa kwa kutumia mbinu kusudio, zikatafsiriwa kwa kutumia tafsiri mawasiliano na kisha kuchanganuliwa kithamano. Ushabihiano wa kimaana wa methali hizi uliangaziwa ili kutimiza madhumuni ya utafiti. Mkabala wa Ufeministi Hakiki wa nadharia ya Uelemea Kike umetumiwa kama kiunzi cha kuchanganulia methali hizi. Makala hii inakusudiwa kutoa mchango adhimu katika nyanja ya fasihi kwa kupanua mawanda ya maandishi yanayohusu methali za Kikikuyu, Aidha, makala hii pia inatarajiwa kuwa kichocheo kwa watafiti ambao wangependa kutalii nyanja zingine za Fasihi Simulizi mbali na kumulika methali kama mojawapo ya vipengele vya utamaduni. Uchanganuzi wa usambamba wa methali hizi umesaidia kubainisha kama jamii hizi zinamkweza au kumkwaza mwanamke. Utafiti huu umebainisha jinsi mwanamke alivyochorwa kitaswira.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/24Mbinu za Kufundisha Kiswahili kama Lugha ya Kigeni kwa Kuzingatia Utamaduni Jamii2025-05-08T08:22:47+03:00Daud Khamisidaudkhamis120@gmail.comNeema Mturoneemamturo@yahoo.comSarah Ngesusarahngesu@gmail.comArnold Msigwaagawasike@gmail.com
Makala hii inachanganua mbinu zinazotumika katika kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni ili kuwezesha uzingativu wa utamaduni jamii. Tafiti mbalimbali zimeonesha mchango wa mbinu za kufundishia lugha kwa wajifunzaji Kiswahili kama lugha ya kigeni. Licha ya kuwepo uhusiano kati ya utamaduni jamii na ufundishaji wa lugha darasani, tafiti hazijaonesha namna mbinu hizo zinavyoweza kutumika ili kuwezesha uzingativu wa utamaduni jamii. Utafiti huu umezingatia mkabala wa kitaamuli. Data zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya usaili huria kwa walimu, na kuchambuliwa kwa kutumia mbinu ya kusimba maudhui. Vituo na taasisi za MS Training Centre for Development Cooperation, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, na Kiswahili na Utamaduni ndizo zimehusishwa. Nadharia ya Umahiri wa Kimawasiliano na Tamaduni Mchanganyiko ya Hall (1992) imetumika katika makala hii. Matokeo yamedhihirisha mbinu zifuatazo hutumika miongoni mwa wafundishaji wa Kiswahili: Matumizi ya teknolojia, mbinu ya uzamaji kindakindaki, mbinu ya maelezo au ufafanuzi, mbinu ya ufaraguzi na mbinu ya vitendo halisi. Kwa hivyo, makala hii inapendekeza kuwa ni muhimu sana katika taasisi na vituo husika kuwa na programu za kuwaelekeza walimu namna bora ya kutumia mbinu hizi ili kuzingatia utamaduni jamii. Vilevile, tafiti mbalimbali zifanyike kuonesha changamoto zinazowakabili walimu katika uzingatiaji wa utamaduni jamii darasani.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/23Usawiri wa Taashira ya Uongozi Barani Afrika katika Tamthilia ya Zilizala2025-05-08T08:03:38+03:00Waithiru Kago Antonymuusyaj@yahoo.com
Makala hii inahusu uhakiki wa usawiri wa taashira ya uongozi katika nchi za Afrika, hasa zile zilizowahi kutawaliwa na mbeberu, kwa kujikita katika tamthilia ya Kiswahili. Tamthilia iliyohakikiwa ni moja ambayo imeandikwa na Kimani Njogu: Zilizala. Nia ya uhakiki huu ilikuwa kujadili namna mwandishi huyu ameusawiri uongozi barani Afrika kitaashira kwa lengo la kuukosoa na kuuelekeza. Makala hii iliongozwa na Nadharia ya Baada ya Ukoloni. Nguzo zilizoongoza uchanganuzi wa data ya makala hii ni pamoja na vita vya uhuru, ukoloni mamboleo, na uzinduzi mintarafu ya kusudi la uhakiki wa makala. Zilizala ilichaguliwa kimakusudi kutokana na maudhui makuu ya uongozi yanayojadiliwa na mwandishi. Kimani Njogu alifanikiwa kulisawiri suala la uongozi katika mataifa mengi barani Afrika, hususani Kenya kwa kutumia kazi ya kifasihi ili kuepuka kukaripiwa na utawala au hata uongozi wowote ule. Suala kuu lililodhihirika katika tamthilia hii ni la ukoloni mamboleo kupitia istilahi ya kitafsida ya utandawazi. Kupitia mhusika Udenda, mwandishi alifanikiwa kutumia mbinu ya taashira kuusawiri uongozi katika nchi za Afrika paruwanja, ingawa kwa njia kwepi na fiche. Mhusika huyu na wengine kadhaa wametumiwa na mwandishi wa tamthilia hii kuwasawiri viongozi wengi barani Afrika, kitaashira, kama vikaragosi vya viongozi wa mataifa ya Japani, Urusi, Uropa na Marekani. Makala hii imedhihirisha baadhi ya mbinu wanazotumia viongozi wa mataifa kwasi na vikaragosi vyao kujinufaisha wao wenyewe huku wananchi katika mataifa tofautitofauti barani Afrika yenye uwezo wa kujiendeleza na kujitegemea wakiendelea kupapatika kwa kusombwa na mawimbi katika bahari la ulofa, ndwele, njaa, na ukame wa kila aina, na hatimaye wanaangamia.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/22Ujitokezaji wa Nomino za Kiswahili Zinazoibua Maana za Kitashibiha katika Riwaya ya Zawadi ya Ushindi na Watoto wa Maman’tilie2025-05-08T07:56:47+03:00Judith Yobujobjudith@gmail.comNeema Mturoneemamturo@yahoo.comSarah Ngesusarahngesu@gmail.com
Makala hii imechunguza ujitokezaji wa nomino za Kiswahili zinazoibua maana za kitashibiha katika riwaya ya Zawadi ya Ushindi na Watoto wa Maman’tilie. Data zilipatikana kwa uchanganuzi matini maktabani kwa usomaji makini wa riwaya teule. Matokeo ya utafii yaliyozaa makala hii yameonesha kuwa nomino ni kijenzi muhimu katika muundo wa kuibua maana ya kitashibiha. Pia, yameonesha kuna nomino za wazi na nomino fiche kwenye kazi za kifasihi zinazoibua maana za kitashibiha. Nomino hizi hutumiwa kwa lengo la kuonesha ubunifu na upekee wa kifasihi ambao wasanii hulinganisha hali za maumbile na tabia za jamii ili kutoa mafunzo, kupamba lugha na kuufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii iliyolengwa kupitia tashibiha. Nomino fiche za makala hii zimeibua maana za kitashibiha kupitia nafasi, muundo na matumizi ya nomino kulingana na muktadha wa sentensi za Kiswahili. Makala hii inapendekeza kuwa wataalamu wa fasihi wanapaswa kuchunguza suala la maana za kitashibiha kwenye tanzu zote za fasihi ili kubaini darajia za maneno hasa vitenzi vinavyobeba dhima za kifasihi na kisarufi katika kuibua maana za kitashibiha ili kusaidia dhana ya fasihi linganishi.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/21Harakati za Ujitambuaji wa Mwafrika katika Tamthiliya ya Kiswahili2025-05-08T07:47:45+03:00Justus Kyalo Muusyamuusyaj@yahoo.comMosol Kandagormosolkandagor@gmail.com
Tamthilia ya Kiswahili ina historia fupi ikilinganishwa na tanzu zingine, hasa ushairi. Tamthilia za kwanza kuwahi kutafsiriwa kwa Kiswahili na zilizoandikwa kwa lugha hii zilizingatia sana maudhui ya kidini, kizalendo, utetezi dhidi ya dhuluma za tawala za kigeni na hasa ukoloni mamboleo. Kinyume na hali hiyo, tamthilia ya Kiswahili katika kipindi cha kuanzia 1950 hadi miaka ya 2020 imesheheni wingi wa tungo zinazosifia Uafrika na heshima ya mtu mweusi hapa barani Afrika na kote ulimwenguni. Uchunguzi wa tamthilia hizi unadhihirisha kujitolea kwa dhati kwa watunzi wake kuelezea, kutetea na kuhimiza heshima ya Mwafrika. Maudhui yake yanakiuka yale masuala mapevu ya utaifa, uraia na tawala za mataifa ya Kiafrika. Kwa sababu hii, makala hii imenuia kuchunguza namna suala la heshima na kujitambua kwa Mwafrika limeshughulikiwa katika tamthilia ya kisasa. Ili kufikia lengo hili, makala imechunguza kwa kina namna suala hili limesawiriwa katika tamthilia ya Mashetani Wamerudi (Mohamed 2016). Tamthilia hii iliteuliwa kwa kutumia mbinu kusudio. Hii ni kwa sababu usomi awali ulionyesha kuwa tamthilia hii imetumia misingi ya nadharia ya Ujumi Mweusi. Data yenyewe ilikuwa ya kitaamuli na ilichanganuliwa vilevile kwa njia ya kinathari. Makala yalionyesha namna ambavyo mwandishi ameweka wazi hadhi ya Mwafrika na kudhihirisha kuwa amejitambua na anapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa na ulimwengu mzima. Hii ni baada ya Mwafrika kuelewa kwamba watu kutoka mabara mengine sio bora kuliko yeye kama ambavyo watu hawa hutaka ieleweke na Mwafrika.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/20Ujumi Unavyoakisi Hali Halisi ya Jamii: Mifano katika Hurafa za Wapemba2025-05-08T07:41:20+03:00Sayfa Abdalla MohammedSayfamohammed03@gmail.com
Makala hii inafafanua ujumi unavyoakisi hali halisi ya jamii katika hurafa za Wapemba. King’ei (2019), akizungumzia kuhusu Ujumi mweusi, ameeleza kuwa ni tangamano la itikadi, falsafa na maoni ambayo yalikusudiwa kutetea hadhi ama utu, uhuru na utamaduni wa Mwafrika. Amesisitiza pia kuwa falsafa hii ilinuiwa kuwa jibu dhidi ya udunishwaji wa Mwafrika katika historia, elimu, dini na falsafa ya Kimagharibi. Kwa kuwa nadharia ya ujumi wa Mwafrika katika kueleza uzuri wa kiidili husisitiza kuwa hakuna uzuri mmoja kwa jamii zote, kila jamii huwa na namna yake na ya kipekee katika kuuthamanisha ujumi kwenye mazingira na nyakati zilizopita. Mhakiki bora wa uzuri wa kiujumi kwa misingi ya idili, anapaswa kuwa ni zao la jamii hiyo au mtu aliyejifunza utamaduni wa jamii hiyo kwa muda mrefu. Pia, kama asemavyo Sanga (2019, uk. 26), vigezo vya kiujumi vya kiidili ni fiche, navyo hutupasa kurejelea kwenye muktadha wa utamaduni wa jamii husika. Kwa njia ya upitiaji na uchambuzi wa nyaraka, makala hii inaonesha ujumi unavyoweza kuiakisi hali halisi ya jamii kupitia hurafa za Wapemba. Tumefafanua kwamba ujumi unaweza kuiakisi hali halisi ya maisha, kupitia vipengele vya kiutamaduni, sanaa jadi/ya za Kiafrika, masimulizi na maudhui ya Kiafrika pamoja na mandhari.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/19Sababu za Kutumiwa U-Nigeria katika Filamu za Kiswahili Nchini Tanzania2025-05-08T07:35:00+03:00Gervas A. Kasigakassiga@gmail.com
Imebainika kuwa filamu za Kiswahili nchini Tanzania ni “pacha” wa filamu za ki-Nigeria. Hivyo, makala hii ambayo data zake zilipatakana kwa kutipia na kuchanganua nyaraka imechunguza sababu zinazowasukuma watayarishaji wa filamu za Kiswahili nchini Tanzania kutumia U-Nigeria katika filamu zao. Isitoshe, kwa muhtasari, makala yamegusia utayarishaji wa filamu za Kiswahili nchini Tanzania kama utamaduni mpya wa vijana wenye harakati za kutafuta nafasi yao kijamii pamoja na kujiongezea kipato. Katika makala, dhana ya U-Nigeria imefafanuliwa kama vijenzi mahususi vya hadithi za filamu za ki-Nigeria vinavyorejelea utamaduni na maisha yao ya kila siku. Aidha, vijenzi hivyo vimebainika kujipambanua katika filamu za ki-Tanzania (Kasiga, 2013; Kasiga, 2018). Zaidi ya hayo, makala imebainisha kuwa, sababu kuu ya kutumika kwa U-Nigeria katika filamu za Kiswahili ni utafutaji wa soko la ndani - Tanzania. Sababu nyingine zilizobainishwa zimehusisha ukosefu wa ubunifu, ukosefu wa nyezo bora za utayarishaji wa filamu, ukosefu wa taaluma ya utayarishaji filamu kwa wasanii, na bajeti hafifu za utayarishaji wa filamu za Kiswahili. Hatimaye, makala imependekeza wasanii wa filamu za Kiswahili ni budi kurudi katika misingi ya fasihi ya Kiswahili kwa kuzichukua kazi mfano za fasihi ya Kiswahili na kuzifanya kuwa filamu. Imebainika kuwa kufanyika kwa jambo hilo kutakuwa ni mwanzo bora wa kuhuisha upya utamaduni wa ki-Tanzania kupitia teknolojia ya filamu.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lughahttp://jadilu.seku.ac.ke/index.php/jadilu/article/view/18Usawiri wa Miiko ya Jadi katika Jamii ya Sasa: Mifano kutoka Jamii ya Wapare2025-05-08T07:21:56+03:00Hatibu Sadihatibusadi@yahoo.comJames Ontierijontieri@gmail.comTigiti S. Y. Sengoprofesasengo45@gmail.com
Ikisiri
Miiko ni sehemu muhimu inayotoa mwelekeo wa mienendo inayokubalika katika jamii yoyote ulimwenguni. Makala haya yanajadili usawiri wa miiko ya jadi katika jamii ya sasa na mifano ikiwa ni kutoka kwa Wapare wa Mwanga Mkoani Kilimanjaro. Lengo kuu la makala haya ni kubainisha namna miiko ya jadi inavyohusiana na kuakisi moja kwa moja maisha ya jamii katika vipengele nuwai vya maisha. Mjadala wa makala haya uliongozwa na swali lililouliza: Miiko kama kipera kimojawapo cha sanaajadiiya inasawiri vipi maisha ya kila siku ya jamii? Mkabala uliotumika kwenye makala haya ni wa kimaelezo. Mbinu zilizotumika katika utafiti wa makala haya ni mbili. Mbinu ya kwanza ni ya usaili ambayo iliwezesha upatikanaji wa data za awali (msingi) na mbinu ya pili ni ya uchanganuzi wa matini ambayo iliwezesha upatikanaji wa data za upili. Nadharia ya Taalimu Ina Kwao na Fasihi Ina Kwao, ndiyo iliyotumiwa kwenye mwendelezo wa uchunguzi na uchambuzi wa makala haya. Matokeo ya tafiti yalionesha kuwa, miiko ya jadi ni kipera muhimu cha sanaajadiiya kilichofumbata tamathali za semi na hurithishwa kwa njia ya masimulizi. Miiko inasawiri maisha ya jamii na ni mhimili muhimu wa maadili. Miiko hiyo huakisi jamii kitamaduni na kimazingira na hivyo kuendelea kudhihirisha umuhimu usio na shaka.
2025-05-08T00:00:00+03:00Copyright (c) 2025 Jarida la Dira ya Lugha